Kilimo Cha Matikiti Maji Kisasa



Kilimo-cha-tikiti-maji
"Kilimo cha matikiti huhitaji udongo wenye rutuba nzuri ulio na virutubisho. Vile vile haihitaji udongo wenye kiasi kikubwa cha tindikali na alikali kubwa. Hali ya udongo katika kipimo cha pH iwe kati ya 6.0 na 7.0. Ingawa mmea una uwezo vile vile wa kuhimili kwenye udongo wenye pH 5.0"


Utangulizi
Matikiti maji hulimwa kama zao la biashara katika sehemu nyingi duniani zenye hali ya hewa ya joto la wastani. Zao hili lina wapatia watu shughuri za kufanya na hivyo kuwapatia kipato kuanzia kwenye nyanja za uzalishaji hadi kwenye matumizi. Matikiti maji ni mojawapo ya jamii aina ya matunda au mbogaboga inayotambaa. Mimea hii inapatikana katika kundi linalojumuisha mimea mingine (curcubitaceae family) kama matango, maboga na maskwash (squash). Zao la tikiti maji ni mojawapo ya zao ambalo lina faida kubwa sana ukilinganisha na mazao mengine kwa muda mfupi. Katika shamba la ukubwa wa ekari moja (1 acre) lililoandaliwa vizuri, kupandwa na kuhudumiwa vizuri mkulima ana uwezo wa kuvuna kiasi cha tani 15-36, ambacho kitamsaidia kupata fedha za kukidhi mahitaji yake mbalimbali na kuondokana na umasikini.

Tikiti-maji

UCHAGUZI WA ENEO
Matikiti maji husitawi katika maeneo yenye joto la wasitani yaani haihimili hali ya joto kali sana, baridi kali, mvua nyingi wala udongo unaotuamisha maji, magonjwa ya fangasi na wadudu waharibifu.

Joto: Matikiti hukua vizuri katika maeneo yenye joto la wastani wa nyuzi kati ya 21 - 30 sentigradi. Iwapo mitikiti itapandwa katika maeneo yenye joto chini ya nyuzi 15 za sentigrade huchelewa kuota.

Mvua: Matikiti maji yanahitaji kiasi cha mvua kati ya millimita 400 - 600 kwa msimu. Mvua nyingi husababisha uwepo wa magonjwa ya fungasi na bakteria ambayo huathili mavuno.

Hali ya Udongo: Kilimo cha matikiti huhitaji udongo wenye rutuba nzuri ulio na virutubisho. Vile vile haihitaji udongo wenye kiasi kikubwa cha tindikali na alikali kubwa. Hali ya udongo katika kipimo cha pH iwe kati ya 6.0 na 7.0. Ingawa mmea una uwezo vile vile wa kuhimili kwenye udongo wenye pH 5.0

Mikoa yaTanzania: Kilimo cha matikiti maji kinakubali vizuri kwenye ukanda wa pwani na miinuko kidogo kama DSM, Tanga, Morogoro, Mtwara, Lindi na Pwani ambapo kuna jua la kutosha. Muda mzuri wa kupanda ni kipindi cha kipupwe mwezi wa tatu mpaka wa tisa.

Uandaaji Wa Shamba
Fyeka vichaka na ng’oa visiki vyote. Katua kwa kina cha sm 22.5 kwenye Sesa. Kabla ya kupandikiza udongo utifuliwe vizuri na majani yaondolewe kabisa. Shamba liandaliwe vizuri kwa kusafisha ili kuondoa mimea mingine ambayo inaweza kuwa ni chanzo cha magonjwa. Weka mbolea ya samadi debe moja kwa kila mita 10 za eneo. Tengeneza matuta katika sehemu ambayo ina majimaji.

Upandaji
Katika shamba la ukubwa wa hecta moja kiasi cha kilo 3 - 4 cha mbegu kinaweza kutumika. Panda mbegu 2 au 3 moja kwa moja katika kila shimo. Usipande katika kitalu kwasababu miche ya mitikiti huwa ni dhaifu sana wakati wa upandikizwaji iwapo itapandwa kwenye kitalu hivyo kupelekea kufa kwa miche hiyo. Panda umbali wa sentimeta 2 chini ya udongo kwa umbali wa mita 1 hadi 2 kutoka shina hadi shina na mita 1.5 - 3 kutoka mstari hadi mstari. Zingatia kutokutumia mbegu za tikiti ulilonunua kwasababu linaweza kuwa ni chotara (Hybrid) ambayo hupelekea kushusha kiasi na ubora wa matikiti yatakayo zaliwa kwa sababu yatakuwa ni kizazi cha pili (F2).

Mbegu: Mbegu maarufu ya tikiti ni Sukari F1, hata hivo madukani zinapatikana nyingi bora na tofauti tofauti.

Upunguzaji Wa Mimea
Mimea ya mitikiti huanza kuota, baada ya kama wiki 2 hivi. Hivyo katika mbegu mbili ulizopanda kata moja na uache ule mche wenye afya zaidi ndio uendelee kukua.

Angalizo: Usinga’oe mche bali ukate ili kuzuia kusumbua mizizi ya mche uliobaki. Vilevile unaweza kupandishia udongo kwenye mashina ili kusaidia kupunguza maji kutuama kwenye mimea yako, pia unaweza kuweka samadi badala ya kupandishia udongo ukiwa na nia ileile ya kuzuia maji yasituame na kuongeza rutuba. Kama una sehemu ndogo ya shamba unaweza kuyawekea matikiti waya wa kutambalia, ila inabidi uwe imara kwa sababu ya kuhimili uzito wa matunda. Wakati mimea inapo anza kutambaa kwenye waya ni lazima uifundishe (kuielekezea) kwenye waya na kuifungia.

Umwagiliaji
Shamba linatakiwa limwagiliwe mara kwa mara wakati mvua zinapokosekana au wakati wa mvua chache. Kipindi muhimu zaidi ambapo mimea hii huhitaji maji ni katika kipindi cha uotaji wa mbegu, wakati wa kutoa maua na siku takribani kumi kabla ya kuvuna. Iwapo kutakuwa na ukosefu wa maji kutasababisha kutengenezwa kwa matunda ambayo si mazuri na yenye umbo baya, pia kupungua kwa ukubwa wa tunda.

Angalizo: usimwagilie matikiti wakati wa jioni sana au usiku kwasababu inaweza kusababisha magonjwa ya majani kutokana na unyevu kukaa muda mrefu. Vile vile usimwagilie juu ya maua wakati wa asubuhi au jioni kwasababu unaweza kuzuia wadudu kama nyuki ambao ni muhimu sana wakati wa uchavushaji.

Uwekaji Wa Mbolea
Weka gramu 65 za NPK/CAN kwa kila mche unapoanza kutambaa. Baadae weka tena gramu 130 kwa mche inapotoa maua.

Matandazo (Mulches)
Matandazo ina maana ya kutumia nyasi na mabaki ya mimea mingine kufunika aridhi. Baada ya miche kutambaaa kwa kiasi unaweza kuweka matandazo (mulches) ambayo yaweza kuwa nyasi kavu kwenye udongo ili kuzuia upotevu wa unyevu vile vile kupunguza uotaji wa magugu shambani kwako. Vile vile matandazo yakioza yanaongeza rutuba kwenye udongo na hulinda udongo dhidi ya mmomonyoko wa udongo.
 
kilimo-bora-cha-tikiti-maji
Matikiti maji shambani

WADUDU NA MAGONJWA
Wadudu wa matikiti wako wa aina mbalimbali na wanaoshambulia sehemu za majani na maua, na wengine hushambulia matunda, pia kuna magonjwa ya fangasi ambayo hushambulia mimea.

Magonjwa kama ukungu wa unga (powdery mildew) na wa chini (Downy mildew) na mengine yathibitiwe kabla hayajaleta madhara kwenye mimea. Ili kujua dawa za magonjwa ni vizuri kuchukua sampuli na kwenda nayo kwenye duka la dawa na pembejeo za kilimo ili kupata dawa sahihi. Dawa aina ya Mancozeb inaweza kutumiwa kuthibiti magonjwa hayo hapo juu.

Vilevile matikiti hushambuliwa na wadudu ambao hukaa katika majani, maua na matunda. Dawa aina ya KARATE itasaidia kuua wadudu wa majani, maua na matunda.
              
KUVUNA NA KUHIFADHI
Matikiti maji ni miongoni mwa mazao yanayochukua muda mfupi sana kukomaa. Kwa kawaida tikiki maji huwa tayari kwa kuvuna baada ya siku 80 hadi 100 baada ya kupanda. Vuna wakati tunda limeiva kabisa. Vuna kwa wakati unaofaa. Epuka kulijeruhi tunda. Hifadhi katika eneo lenye ubaridi nyuzi 15 hadi 20 C. Hifadhi vizuri, unyevua-anga (humidity) uwe 80 hadi 85%. Uza mara tu baada ya kuvuna shambani.

Comments

Related posts